Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
AG FELESHI AELEZA MANUFAA YA MAWAKILI WA SERIKALI KUJISAJILI KATIKA MFUMO WA OAG-MIS
service image

AG FELESHI AELEZEA  MANUFAA YA   MAWAKILI WA SERIKALI   KUJISAJILI

Na Mwandishi Maalum

Dodoma

Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Mhe. Jaji Dk. Eliezer Feleshi  amesema,  usajiri wa    mawakili wa serikali katika  mfumo wa  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  unaojulikana  kama  OAG-MIS  ni zoezi  endelevu na hivyo kuwataka wale ambao  bado hawajajisajili  kuendelea kufanya hivyo.

Akizugumza hivi karibuni    mbele ya  Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dk. Damas Ndumbalo  (Mb)  AG  Feleshi  amesema  usajili  wa mawakili  hao wa serikali walio katika utumishi wa umma, unalenga pamoja na mambo  mengine kuwatambu wapi walipo na wanafanya nini

Amesema,  zoezi hilo  na ambalo  hakudhani kwamba lingekuwa  gumu hasa kutokana na  kwamba  bado kuna  mawakili wengi  wanasuasua kujisajili katika mfumo huo.

Hadi kufikia tarehe 27April jumla ya  mawakili wa serikali 1943  walikuwa wamejisajili kwenye mfumo huo na  kati ya hao  ni 1100 tu ndiyo waliokuwa wamejaza taarifa  zao kwa ukamilifu.

 Pamoja na  kuwatambua lakini pia ni  zoezi  ambalo litaiwezesha  Ofisi yake    kutambua  Mawakili hao  wanatekeleza  majukumu  gani,  ukubwa  wa majukumu au uchache  wa majukumu,sifa na  uwezo wao.

AG Feleshi amebainisha  kwamba,  usajili huo pia utasaidia sana kuangalia  namna bora  ya kuwatumia   mawakili hao katika maeneo mbalimbali kulingana na  sifa na uhitaji, lakini pia kuwaongezea majukumu kwa wale ambao majukumu yao ni machache

Vile vile usajili huo utawawezesha Mawakili hao  walio katika utumishi wa umma kutambuliwa na mamlaka mbalimbali  ikiwamo  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mahakama na kuorodheshwa  kwenye Gazeti la Serikali.

Aidha upatikanaji wa takwimu za Mawakili hao kutaiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kujua namna ya kuboresha huduma za  Sheria hapa nchini  ili kuendana na  wakati na mabadiliko yanayoendelea nchini na duniani kote.

Mwanasheria Mkuu ametoa rai kwa     mawakili hao wa serikali  katika  utumishi wa umaa kuacha kuwa nyuma nyuma katika masuala na mambo yanayowahusu. Na kwamba kwa wale ambao watashindwa kujisajili bila ya kuwa na sababu za msingi watakosa kutambulika, watakuwa wamekiuka sheria na watachukuliwa hatua.

 

 

27 Apr, 2022
Maoni