Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
CHAMA CHA MAWAKILI WA SERIKALI NA CHAMA CHA MAWAKILI TANGANYIKA KUSHIRIKIANA
service image

Na Mwandishi Wetu

Mtumba-Dododma

 

Rais wa Chama cha Mawakili  Tanganyika ( TLS)   Profesa Edward Hosea  amesema  Chama chake  kipo tayari kushirikiana  na kufanya kazi kwa karibu  na  Chama cha Mawakili wa Serikali  (TPBA).

Ameeleza nia  hiyo  jana  alhamisi (Desemba 22,2022)  wakati  alipokutana na  kuwa na mazungumzo na Uongozi wa Mpito wa Chama cha Mawakili wa Serikali  ( TPBA) uliokwenda  kujitambulisha kwa Uongozi wa  TLS .

Profesa Hosea amelitaja eneo ambalo  TLS na TPBA wanaweza kushirikiana  kama likiwekewa mpango mkakati  mzuri  ni  eneo la utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria  kwa wananchi.

Akiongea na  mwandishi wa Habari hii,  Katibu wa  TPBA Bi. Sia Mrema  amesema Rais huyo wa TLS   pamoja na kushukuru kwa Uongozi wa TPBA kuona haja na umuhimu wa Kwenda kujitambulisha kwa uongozi wa TLS  pia alionyesha nia ya wazi kabisa ya vyama hivyo kushirikiana kati baadhi ya maeneo ambayo vyama hivyo vinashabihiana likiwemo  hilo la  utoaji wa msaada wa kisheria kwa wananchi.

Bi. Mrema  amesema    TPBA  imeona na kukubaliana juu  ya wazo hilo  la kushirikiana katika utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria ingawa kimsingi Wizara ya Katiba na Sheria  ndiyo inayosimamia huduma  hiyo lakini  Vyama hivyo vina idadi kubwa ya Mawakili  licha ya kuwa vinatekeleza  majukumu yao katika mazingira  tofauti.

Katibu  huyo wa TPBA alibainisha  Zaidi kwakusema,  “Tumekwenda kujitambulisha kwa wenzetu na  tumepokelewa vizuri sana na kwa kweli  wao wamefarijika kwa sisi  Kwenda kujitambulisha na sisi  tumefarijika kwa namna tulivyopokewa  lakini kubwa Zaidi kuwa  na  mazungumzo yenye tija”,

Akasema  uongozi  wa TPBA  ulitumia ziara hiyo kuelezea kwa ufupi Taarifa ya TPBA na uwepo wake na nia ya kuwa na ushirikiano  wa karibu na TLS katika baadhi ya  maeneo. “Tulikuwa na majadiliano ya kina  kueleza taarifa fupi ya Chama chetu na kwamba tupo , lakini pia kuona   namna gani  tunaweza kuwa  na  ushirikiano katika baadhi ya  maeneo” akasema Bi. Mrema

Na kuongeza kuwa eneo moja wapo ambalo wamekubaliana kuliwekea mpango mkakati ni katika eneo  la utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi.

Kwa  mujibu wa  Bi.  Sia Mrema eneo  jingine ambalo wamekubaliana kuangalia namna ya kushirikiana ni  katika eneo la uhuishaji  wa taarifa za mawakili  wa serikali katika  Kanzi Data ya TLS inayofahamika kama Wakili Data Base  pamoja  na kubadilishana uzoefu katika maeneo  mengine.

Kuhusu  sjuala Uhuishaji wa taarifa  za wanachama kutasaidia pamoja na  pamoja na  masuala mengine  kutasaidia kufahamu wanachama walio hai hususani  mawakili wa Serikali.

Vyama hivyo pia  vimekubaliana  kuona namna gani  mifumo ya kanzi data  ya OAG-MIS na Wakili Data Base   itakavyoweza kusomana katika baadhi ya  maeneo. Na kuongeza kuwa tayari wataalamu wa TEHAMA wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TLS wameanza mawasiliano.

Katibu wa TPBA ameeleza  pia kwamba  waliwasilisha ombi kwa uongozi wa TLS la kuomba  Mawakili wa Serikali  ambao wapo  katika orodha ya wanaodaiwa ada za TLS wasiondolewa katika kanzi data kwanza  ili uongozi wa TPBA uone namna ya kulishughulikia tatizo  hilo.

Wakijibu ombi hilo  Uongozi wa TLS umeushauri  uongozi wa TPBA kuandika  barua rasmi  kuhusiana na  suala hilo.

Chama cha Mawakili wa Serikali kilizinduliwa rasmi   na  Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan  wakati wa Mkutano Mkuu  Maalum wa  Mawakili  uliofanyika Septemba 29,2022 Jijini Dodoma.

mwisho

23 Dec, 2022
Maoni