Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
MABARAZA YA WAFANYAKAZI NI CHOMBO MUHIMU MAHALI PA KAZI-WAZIRI NDUMBARO
service image

MABARAZA YA  WAFANYAKAZI NI CHOMBO MUHIMU MAHALI PA KAZI-WAZIRI NDUMBARO

Na Mwandishi wetu

April 22 mwaka huu,  Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dk. Damas Ndumbaro alikuwa mgeni rasmi katika Baraza la Wafanyakazi la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Baraza hilo lilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa jengo la  Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Jiijni Dodoma na  Mwenyekiti wake akiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dk. Eliezer Feleshi.

Ajenda  kuu ya  baraza hilo ilikuwa ni  kupokea na kujadili taarifa ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Waziri Ndumbaro katika hotuba yake ya ufunguzi wa baraza hilo, pamoja  na  kupongeza kwa uhai wa baraza la wafanyakazi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  pia alipongeza  kwa namna Menejimenti ya  Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kwa  kutekeleza jukumu la kisheria la kuwashirikisha watumishi kwenye mipango ya uendeshaji wa Taasisi.

Anasema, hatua hiyo  ni njema, kwa sababu kila palipo na watumishi wengi pana mawazo mengi na hivyo ushirikishwaji kuhusu mipango ya uendeshaji  wa Ofisi kunasaidia  kupata mawazo shirikishi yanayorahisisha uendeshaji  na  pia  ni fursa ya kusikiliza changamoto mbalimbali  zinazowakabili watumishi.

“Katika vikao  hivi ( Baraza La Wafanyakazi) ndiko  tunapopata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili  watumishi, lakini pia watumishi wanapata  morali ya kazi  kama wanashikiri  katika kuandaa na utekelezaji wa mipango ya Taasisi”.  Amesema Waziri  na kuongeza

“Hivyo, pamoja  na kuwapongeza kwa hatua hii, ninatoa rai muendelee kufanya  vikao kama hivi kama ilivyopangwa ili  kudumisha pamoja na mambo mengine mahusiano mazuri baina ya Uongozi na Utumishi”. Akasisitiza Waziri wa Katiba na Sheria.

Akimkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria kufungua  Baraza hilo, Mwenyekiti wa   Baraza   Mwanasheria Mkuu wa Serikali   Mhe Jaji Dk. Eliezer Feleshi, aliwaeleza wajumbe wa Baraza kwamba,    ukomo wa bajeti umeongezeka kutoka kiasi cha shilingi bilioni tano na milioni ishirini na mbili, mia tisa themanini na moja elfu ( Tshs 5,022,981,000) zilizotengwa mwaka wa fedha 2022/2023 hadi kufikia ukomo wa kiasi cha shilingi bilioni sita na milioni mia tisa ishirini na nne mia tisa kuma na nane elfu ( Tshs. 6,924.918,000/=) kwa  mwaka wa fedha 2022/2023.

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  ongezeko hilo ni wazi  linalenga kuiongezea uwezo  Ofisi ya Mwanasheria  Mkuu wa Serikali  katika utekelezaji wa majukumu yake kwenye  mipango iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha.

“Natoa rai kwa watumishi wote  wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  kuongeza ubunifu na mikakati  kabambe ili kutekeleza kazi za Ofisi kwa weledi wa hali ya juu” amesisitiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Baadhi ya wajumbe wa Baraza  waliopata fursa ya  kuchangia wasilisho la taarifa ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 ya  Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, walielezea kuridhishwa kwao na namna ambavyo wamekuwa wakishirikishwa na  kushiriki hatua kwa hatua katika kuandaa bajeti hiyo.

27 Apr, 2022
Maoni