Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
MAJALIWA AWATAKA WATUMISHI WA OMMS KUENDELEA KUCHAPA KAZI KWA BIDII
service image

NA MWANDISHI WETU

MTUMBA-Waziri  Mkuu  Mhe.  Kassim Majaliwa leo ( Jumatatu) amefanya ziara ya kutembelea na kukagua  maendeleo ya  ujenzi wa Majengo ya Wizara na Taasisi za Serikali . Majengo   hayo  yanajengwa katika  Mji wa Serikali  eneo  la Mtumba  Jijini Dodoma

Miongozi  mwa  Majengo  aliyotembelea   Waziri  Mkuu  ni  Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  ambapo akiwa katika eno hilo  alipokelewa na  Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria  Kamishna Msaidizi  Neema Mwanga,    Naibu  Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Dkt. Evaristo Longopa, Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu N Mabele   pamoja na Wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Akiwa katika eneo la ujenzi la Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa  Serikali,  Waziri  Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa   akiwa ameongoza na  Waziri wa Nchi Ofisi ya   Waziri Mkuu, Sera,   Bunge na Uratibu,  Mhe Jenista Mhagama , Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi. Rosemary Senyamule  na viongozi wengine  alitoa  maagizo mbalimbali  kwa  Uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu  wa Serikali ,  watumishi wa Ofisi hiyo na   Mkandarasi SUMA JKT.

Baadhi ya  maagizo  aliyoa  Waziri Mkuu  ni  pamoja na kumtaka Mkandarasi SUMA JKT kuongeza kasi  ukamilishaji  kazi mbalimbali zinazoendelea na ikibidi kuanza sasa kazi   usiku na mchana.

Akasema “ Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi ameiamini   SUMA JKT kujenga mradi huo, na kwa sababu hiyo yeye ( Waziri  Mkuu) hategemei SUMA JKT  ikawa  ni ya mwisho  katika kuukamilisha mradi huo. Meja Jenerali( Mkuu wa JKT)   upo hapa ni  mategemeo yetu kazi  itakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa”

Akasema  kukamilika kwa jengo hilo siyo tu kutawafanya  watumishi wote wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa katika jengo moja, lakini pia kutarahisisha upatikanaji wa huduma ambazo  zote zitapatikana katika jengo  hilo. Na  akawataka  wafanyakazi wa OMMS kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

Waziri  Mkuu ambaye alionyesha pia kuridhishwa kwake  na hatua za maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo ambalo mpaka sasa limefika  asilimia 65 alikuwa na haya ya kusema.

“Nimefika hapa kutembelea na kuona maendeleo ya ujenzi wa majengo haya ya serikali  na taasisi na  kote nilipopita nilichoelewa ni utofauti  wa hatua  mbalimbali za ujenzi  wa majengo haya. Hapa  mmefikia asilimia 65 ni  jambo  nzuri, lakini  matarajio yetu ni kwamba jengo hilo litakamlika kwa wakati”.

Akabinisha  kwamba lengo la  serikali  ni kuhakikisha  kwamba  ifikapo   Januari 2024 watumishi wote wa serikali  watakuwa wameshahamia katika majengo hayo mapya.

Aidha akasema  katika kipindi cha  miezi mitatu ya mwisho  wa mwaka huu   itakuwa ni  ukamilishaji wa mahitaji mbalimbali zikiwamo  fanicha na  mambo mengine ya msingi.

Akizungumzia Zaidi  kuhusu ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi huo,  Waziri Mkuu ametoa wito  kwa Viongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na watumishi wa Ofisi hiyo kuhakikisha wanapita mara kwa mara kukagua kazi  zinazoendelea ikiwa ni pamoja na kubaini  changamoto zinazojitokeza.

“Viongozi   katika ngazi mbalimbali  jitahidi kufuatilia na kupita mara kwa mara kuangalia  maendeleo ya  ukamilishaji wa mradi,  hata  wafanyakazi mnao wajibu wa kupita  na kujionea  kazi zinazoendelea kwa maslahi ya Serikali lakini pia wananchi waweze kuona kodi zao  zimetumikaje   kwa kukamilika kwa  majengo haya” akasisitiza Waziri Mkuu.

Akizungumzia kuhusu uagizaji wa  baadhi  ya  vifaa  vya ukamilishaji wa majengo hayo  kutoka nje kama vile   vigae, (tiles)  Waziri  Mkuu amewashauri watendaji wa  Wizara na Taasisi pamoja na Wakandarasi   kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya  ndani.

Amesisitiza kuwa  haitakuwa jambo jema na si sahihi kuagiza bidhaa kutoka nje ya nchi ili hali kuna viwanda vinavyozalisha bidha hizo hizo hapa nchini.

Akasema  kwa kuangiza bidhaa kutoka nje, kwanza, kunaua viwanda vya ndani ambavyo serikali imekuwa ikivipigia debe na kukaribisha wawekezaji,  lakini   ununuzi huo pia unaodosha fedha za kigeni  kwenda nje  na kupunguza mzunguko wa fedha.

“Nikiwa pale  Wizara ya Ardhi   nimeambiwa makontena ya vigae yanasubiriwa kutoka Ujerumani na Uturuki,  nikashangaa sana  kwa nini  waagize Ujerumani na Uturuki wakati  tunavyoviwanda vya viage ( Tiles ) kule  Mkuranga na   Chalinze  je viage hivi vya ndani  havina ubora mpaka muagize kutoka  nje?” Akahoji Waziri  Mkuu

 Na kuongeza  “ lazima  tubadirishe muelekeo, hivi wizara zote  na taasisi zote zikiagiza bidhaa  kutoka nje ni kiasi  gani cha fedha za kigeni  kinakwenda nje, na je  viwanda vya  ndani  havitoshelezi mahitaji,  hili ni lazima tuliangalie upya  kama sisi wenyewe hatutanua bidhaa za viwanda  vyetu  vya ndani ambavyo tunavipigia debe sana je majirani zetu watatuonaje” akahoji tena Waziti Mkuu.

Akasema  Serikali   imekwisha kuaanda fedha kwaajili ya  ukamilishaji wa majengo hayo na kuwataka  viongozi kufuatilia.

Awali   Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Dkt. Evaristo Longopa alitoa  maelezo mafupi  kuhusu  maendeleo ya mradi huo.

Imeandaliwa na  Kitengo cha Mawasiliano

3/7/2023

 

03 Jul, 2023
Maoni