Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
MENEJIMENTI YA OMMS YARIDHIA MICHORO YA JENGO LA ARUSHA
service image

Na Mwandishi Wetu

Mtumba,Dodoma

Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  jana jumatano (Desemba 21,2022) imeridhia michoro ya ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoani   Arusha.

Kuridhiwa kwa michoro hiyo  na Menejimenti kumetokea baada ya  Wataalamu kutoka  Wakala wa Majengo ( TBA)kuwasilisha nyaraka mbalimbali  ikiwamo michoro ya mradi huo  pamoja kuelezea hatua kwa hatua za  mchakato mzima wa maandalizi ya eneo  la ujenzi.

Akielezea  mchakato mzima ulivyokuwa na utakavyokuwa katika  utekelezaji wa mradi huyo ,  Mhandisi Juma Dand ambaye ni Kaimu Wakala wa  Majengo Mkoa wa Arusha, alibainisha kuwa   TBA kama  mshauri mwelekezi imezingatia masuala yote ya  msingi yakiwamo yanayohusu masuala ya mazingira na  matumizi endelevu ya ardhi  kwa kukutana   na kuwa na vikao na wadau  mbalimbali.

Mhandisi  Dand akatumia  fursa hiyo pia kuushukuru uongozi wa Ofisi ya Mwasheria Mkuu wa Serikali  kwa kuendelea kuimaini  Taasisi na kuipa kazi ya kuwa  mshauri  mwelekezi wa mradi Arusha.

Katika  maelezo yake kwenye  kikao hicho ambacho kilikuwa chini ya Uenyekiti wa Kaimu  Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Bw. Onorius Njole , Mhandisi  Dand alitaja baadhi ya matakwa ambayo yapaswa kuzingatiwa ni pamoja  kulinda  mazingira ya mto unaopita  katika eneo  la mradi.

Kwa upande wake Kaimu Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Njole   amewashukuru wataalamu hao wa TBA   kwa kazi ya maandalizi ya mradi  huo  pamoja na  ufafanuzi walioutoa  kutokana na maswali  yaliyoulizwa na wajumbe wa kikao.

“Tunawashukuru kwa kuja kwenu na  kwa maelezo  na ufafanuzi mliotoa, tunaridhia  pamoja na   michoro mliyotuonyesha lakini pia  kuna mapendekezo  machache tuliyotoa basi mtaangalia  namna gani ya  kuyafanyika kazi”. Akasema Bw. Njole.

Kikao hicho  cha  Menejimenti kilihudhuriwa  pia na Maafisa Waandamizi kutoka   Divisheni na Vitengo vya OMMS.

Kiwanja cha  Mraji wa Jengo la Ofisi ya Mwanasheria   Mkuu wa Serikali   kina ukubwa  wa mita za mraba 2901 na kipo  katika  barabara ya Arusha- Moshi kati ya Hoteli ya  Mount Meru na  Pan  African Postal  Union na umbali mfupi kutoka ilipo  Mahakama Kuu.

Jengo  la Arusha ambalo  ramani  yake  inafafana  na jengo la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali  mkoani  Mwanza na litakuwa Jengo  Jumuishi la Taasisi za Kisheria kama ilivyo Mwanza.

Taasisi   za Kisheria zitakazotumia Jengo  la  Arusha ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Kabidhi Wasii  Mkuu.

WAKATI HUO HUO,  leo ( alhamisi) Bodi ya Ununizi ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali    imepitisha njia ya  manunuzi  kwaajili ya kumpata Mkandarasi atakayejenga  jengo la Arusha.

Bodi hiyo  ilikutana chini ya Kaimu  Mwenyekiti  Bw. Buji Bampebuye imefanya kikao chake katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ipagala.

Mwisho

22/12/2022

 

 

22 Dec, 2022
Maoni