Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
TAASISI ZA KISHERIA ZIACHWE ZIJIPANGIE MAMBO YAO- AG FELESHI
service image

Na  Mwandishi Maalum

28/11/2022

MWANZA

Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Mhe. Jaji Dkt.  Eliezer Feleshi amesema,  ifikie mahali sasa   kwa Taasisi za Kisheria  nchini  ziachwe zijipangie mambo yao kwa  namna zinavyoona badala ya kupangiwa.

Amesema ni kwa  kujipangia mambo yao  na mipango yao ndipo  Taasisi hizo  zitakayoweza kwa ukamilifu na kwa tija  kuisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

 Kwa sababu hiyo Dkt Feleshi,  amezihimiza  taasisi hizo ambazo ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zianze  zenyewe  kujisahihisha na kutorudia makosa ya nyuma ya kupangiwa  mambo yanayohusu  majukumu yao.

“ Kama binadamu tunaishi kwa kujisahihisha , na kujisahihisha si  vibaya  kwa sababu ni kwa kujisahihisha  unakuwa na hamu ya kwenda mbali sana. Kwa hiyo sisi kama Taasisi za kisheria tunapaswa kujisahihisha ili tusirudie makosa ya nyuma ya kutojipangia mipango yetu  tunavyotaka wenyewe  na kuimilika mipango hiyo”. Amesisitiza  AG Feleshi

Alikuwa akifungua kikao  Jumuishi   cha Menejimenti  kutoka Taasisi hizo  tatu,  kikao  ambacho, pamoja na  Mwanasheria Mkuu wa Serikali   kimehudhuriwa pia na    Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya  Mashtaka, Bw. Sylvesta Mwakitalu na  Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Bonifance  Luhende.

Kikao hicho   kimepokea na  kujadili taarifa ya maendeleo ya  Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali . Kikao kimefanyika katika  Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya  Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

.

Pamoja na  kusisitiza  umuhimu wa taasisi hizo tatu kujisahihisha na kutorejea makosa ya nyuma,   amesisitiza pia haja na umuhimu  kwa taasisi hizo tatu kuwa na  uwajibikiaji wa pamoja bila kuathiri nafasi au majukumu ya kila Taasisi .

“Uwajibikaji wa pamoja utahakikisha  Taasisi hizi zote zinafanikiwa kwa pamoja katika utekelezaji wa majukumu  yao, tukiwa na uwajibikaji wa pamoja na ushirikiano wa pamoja tutakuwa na sauti ya Pamoja na tutakuwa na nguvu kubwa ya kuisaidia serikali ” akabainisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka.

Kwa upande wake , Mkurugenzi  Mkuu wa Mashtaka ( DPP) Bw. Sylvesta  Mwakitalu yeye amesema,   Taasisi hizo tatu  ni taasisi  muhimu   sana katika kuhakikisha  haki, amani na maendeleo ya taifa  la Tanzania.

“ Wote  tunafahamu  umuhimu wa Ofisi hizi Tatu kwa maendeleo na ustawi wa nchi  yetu. Kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikilegea, ikiwa watumishi wake hawatatimiza majukumu yao kwa makusudi  au kwa bahati mbaya au kwa uzembe mnajua madhara yake ni nini kwa Serikali” akasema DPP Mwakitalu na  kuongeza

“Kama Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali  ikilegalega katika utekelezaji wa majukumu yake   sote tunajua namna gani maamuzi yanayotolewa  na  mahakama  yatakavyowaumiza watanzania.

Akaoongeza “Ofisi ya Mataifa ya Mashtaka  tusipofanya kazi yetu  ipasavyo hakutakuwa na amani,  biashara hazitafanyika, uchumi hautakua  lakini pia nchi haitakalika.

Kwa sababu hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka amesema  anafurahishwa sana na  namna ambavyo Taasisi hizo  tatu zimeanza kuwa na mashirikiano na  mahusiano  ya karibu katika utekelezaji wa  majukumu yao.

“Hiki ni  kikao cha kihistoria, ninaona mwanga mpya tukitumie kikao hiki  kujadiliana  namna bora ya utekelezaji wa majukumu yetu kikoa ambacho  kitatupa mwelekeo wenye tija  kwa taasisi zetu na  watumishi wake kwa ujumla

Naye Wakii Mkuu wa Serikali  Dkt Bonifance  Luhende  naye    akizungumzia  kuhusu kikao    jumuishi  cha Menejimeti za Taasisi hizo tatu,  amesema,  kikao hicho kinafanyika  wakati muafaka na kitatoa fursa  ya kujadili changamoto   mbalimbali zinazoikabili  Taasisi hizo.

“Jukwaa hili linatupa fursa ya kujadili na  kutathimini hali ilivyo sasa katika taasisi zetu,  hali ya utekelezaji wa majukumu yetu,  hali ya   watumishi wetu je hali zao zinaendana na majukumu  makubwa na mazito wanayoyatekeleza,  jukwa hili  litufanya tuwe na sauti moja na Kwenda kama kundi moja”. Amesitiza Dkt.  Luhe

Pamoja na Viongozi Wakuu wa Taasisi hizo,  viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni  Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo  Longopa, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali  Bi. Sara Mwaipopo na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Joseph Pande, Wakurugenzi, Wakurugenzi wasaidizi,  Wakurugenzi wa Mipango, Wakuu wa Vitengo vya Manunuzi na Wataalamu wengine kutoka  Taasisi hizo  tatu.

Wakati huo huo  Waziri  wa Katiba na Sheria  Dkt. Damas  Ndumbaro  kesho ( Jumanne) ataweka Jiwe la Msingi  la Jengo  la Kituo   Jumuishi  cha Taasisi  za Kisheria.

Jengo hilo   linajengwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika eneo la Buswero   Mkoani  Mwanza na litahudumia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,  Ofisi ya Taifa ya Mashtaka,  Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na RITA.

28 Nov, 2022
Maoni