Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali
WANASHERIA EACOP WAMTEMBELEA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
service image

  WANASHERIA  EACOP WAMTEMBELEA  MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki  Feleshi amekutana na kufanya  mazungumzo  na Bw. Stanley Mabiti, Meneja Sheria wa Mradi wa Bomba la  Mafuta la  Afrika Mashariki ( EACOP).

Mazungumzo  kati ya  Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali  na Bw. Mabiti yamefanyika  jana  tarehe 12/12/2022   katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jijini  Dar es Salaam. Mazungumzo  yalihudhuriwa pia  na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniface Nalija Luhende. 

Bw.  Mabiti aliambatana na Mshauri wa Sheria  wa mradi huo  (EACOP) Bw.  Yohana Mganga    ambao waliomba  kuonana na    Mhe. Jaji Dkt. Feleshi kwa  madhumuni ya kufahamiana naye na kumfahamisha masuala mbalimbali yanayohusiana na  maendeleo ya mradi huo wa EACOP.

Meneja Sheria wa EACOP Bw. Mabiti pia aliwasilisha hoja juu ya haja ya kufanyika warsha  ya kuzijengea uelewa wa pamoja Taasisi zote za Serikali zinazohusika katika   utekelezaji  wa Mkataba wa Nchi Hodhi za Mradi wa Bomba hilo la Mafuta.

Kwa upande wake,  Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Feleshi aliwashukuru wataalamu hao  kwa kumtebelea  na kubadilishana naye mawazo kuhusu utekelezaji  wa mradi huo ambao ameutaja kuwa wenye Tija kwa Taifa.

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashari ni  Mradi Shirikishi kati ya Tanzania na Uganda ambapo  bomba hilo linajengwa kuanzia Kabale-Hoima Nchini Uganda hadi Peninsula ya Chongolani Mkoani Tanga Nchini Tanzania.

Mradi huo  una urefu wa jumla ya kilomita 1443 ambapo kati ya hizo, kilomita 296 zipo nchini Uganda  na  kilomita 1147  zipo nchini Tanzania.

Lengo la Mradi huu ni kuwezesha mafuta yatakayozalishwa nchini Uganda kusambazwa katika  soko la ndani na sehemu itakayosalia kuuzwa nje kwenye soko la  Kimataifa  kupitia bomba hilo.

Mwisho.

Maura Mwingira

Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano Serikalini

13/12/2022

 

 

13 Dec, 2022
Maoni